Wednesday, March 21, 2012

Madaktari kutoka Muhimbili kutoa Elimu ya Afya na Vipimo Bure kwa Wanamichezo wa Namanga Jogging & Sports Club Jumapili Machi 25

Katibu Mkuu wa Namanga Jogging S.C, Andrew Mangole
Na John Badi

Jopo la Madaktari kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Jumapili Machi 25.2012, linatarajia kutoa elimu ya afya, tiba na vipimo bure kuhusu Saratani ya Kibofu cha Mkojo kwa wanamichezo wa Klabu ya Namanga Jogging Sports.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Katibu Mkuu wa Klabu ya Namanga, Andrew Mangole imesema kuwa lengo kuu la mafunzo hayo ni kuwafanya wanamichezo kulielewa vizuri tatizo hilo la Saratani ya Kibofu cha Mkojo ili kuepuka upasuaji.

Aidha taarifa hiyo imesema kuwa kabla ya zoezi hilo, wanamichezo wa Namanga Jogging S.C wataungana pamoja na klabu zilizoalikwa za Kunduchi Kwanza Jogging S.C, Biafra Jogging S.C na Kawe Jogging S.C,  katika kukimbia pamoja 'jogging' asubuhi.

Taarifa ya Bw. Mangole inabainisha zaidi  kuwa zoezi la utoaji wa elimu hiyo, walengwa wakuu watakuwa ni wanamichezo wote hususani wa jinsia ya Kiume  wenye umri kuanzia miaka 40 na kuendelea kwani rika hilo ndilo hukumbwa sana na matatizo ya saratani ya kibofu cha mkojo.

Pamoja na kuwa walengwa wakuu ni wanamichezo lakini klabu ya Namanga Jogging imeona ni vyema kuwashirikisha watu wengine ambo si wanamichezo kuja kupima afya zao kwani huduma hizo zitatolewa bure bila gharama yeyote.

No comments:

Post a Comment